Mwandishi na mwalimu maarufu wa Kiswahili, Ruo Kimani Ruo. Picha/Hisani
Na Wanderi Kamau
Jumuiya ya Kiswahili nchini Kenya inaomboleza kifo cha ghafla cha mwandishi, msomi na mwalimu maarufu wa Kiswahili, Ustadh Ruo Kimani Ruo.
Kulingana na taarifa kutoka kwa familia yake, Bw Ruo alifariki mnamo Alhamisi, Novemba 27, 2025, baada ya kuugua.
“Ni kwa masikitiko makubwa tunawatangazia kifo cha Ruo Kimani-Ruo, aliyefariki mnamo Novemba 27, 2025. Alikuwa mume, baba, babu, ndugu, mjomba na rafiki, ambaye kifo chake kimewasikitisha wote waliomjua,” ikasema familia yake.
Bw Ruo alikuwa mwalimu na mwandishi wa miaka mingi anayesifika kwa kuchangia ukuaji wa Kiswahili kupitia uandishi wa makumi ya vitabu na makala ya gazeti, hasa gazeti la Taifa Leo.
Mwandishi wa vitabu
Baadhi ya vitabu alivyoandika ni: Kaida za Uchanganuzi: Utanzu wa Ushairi, Wasakatonge na Hadithi Nyingine, Kiburi cha Nondo na Hadithi Nyingine, Bahasha ya Urithi na Hadithi Nyingine (zote zikiwa mkusanyiko wa hadithi fupi) kati ya vingine.



Bw Ruo alikuwa mshiriki wa kundi la WhatsApp la Ukumbi wa Kiswahili, linalowajumuisha wasomi, wanahabari na wakereketwa maarufu wa Kiswahili nchini na sehemu nyinginezo, ambapo alikuwa akitoa michango muhimu kuhusu masuala tofauti ibuka ya kiusomi, yanayohusu ukuaji wa Kiswahili.
Magwiji wamwomboleza
Wakiomboleza kifo chake, magwiji tofauti wa Kiswahili walimtaja kama mtu muungwana, mwadilifu, mnyenyekevu, mwenye roho safi, aliyetangamana virahisi na kila mtu.
Prof Clara Samiji Momanyi: “Poleni sana jamaa na marafiki wa marehemu. Mungu amlaze pema.”
Mwalimu Alex Ngure: “MAKIWA! Pumzika kwa amani Ustadh Ruo Kimani Ruo.”
Vikita Yusufu: “We! Makiwa! Inasikitisha.”
Atulo Francis: “Makiwa kwa ndugu na jamaa zake Mstahiki Ruo. Hakika kuondoka kwako kunaacha masikitiko makubwa. Eewe Mola ijalie familia yake rehema kuweza kukabiliana na mauko haya. SALAMA.”
Mwalimu Enoch Nyariki: “Makiwa kwa wote ambao umewasibu msiba. Mungu awape nguvu za kukikabili kipindi kigumu cha kumwomboleza Ustadh Ruo Kimani.”
Mwandishi Amiri Swaleh: “Innaa lillahi wa innaa ‘ilaihi raaji’un. Mungu ailaze roho yake pema.”
Soma zaidi: Kiswahili fraternity mourns Prof John Habwe
Profesa Iribe Mwangi, Chuo Kikuu cha Nairobi: “Oh! Makiwa! Rambirambi zangu kwa jamaa.”
Profesa Kithaka wa Mberia: “Pole kwa jamaa na marafiki za Ruo Kimani Ruo. Mungu aiweke roho yake aziwekapo roho za wema na awape jamaa zake Subira.”
Bitugi Matundura, ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Chuka, alirejelea safari na mwingiliano wake wa kiusomi na Bw Ruo kabla yake kufariki.
“Taarifa za kusikitisha na kuhuzunisha sana. Si zamani sana, Ustadh Ruo Kimani Ruo alinipigia simu. Alihitaji kwa dharura picha ya mwandishi wa tamthilia, Bw Henry Kuria – mtunzi wa : Nakupenda Lakini …/. Alinifahamisha kwamba kuna mradi alikuwa anaufanya na Prof Mugyabuso Mulokozi, ambapo waliihitaji picha hiyo kwa dharura. Niliwasiliana na wahariri wa Taifa Leo, Chris Adungo na Steve Musamali. Nao wa ukarimu wao, wakaisakura maktaba ya Nation Media Group. Walipata picha ya HK iliyochapwishwa kwenye makala ya gazeti. Wakanitumia, nami nikamtumia Ustadh Ruo Kimani Ruo. Akafurahi ghaya ya kufurahi. Undugu chambacho wahenga, ni kufaana. Nilikuwa ninarudisha mkono, kwa wema alionitendea, kunitumia – kwa dharura baadhi ya vitabu nilivyovihitaji kwa gharama zake. Vitabu hivyo kavipokea Dkt Ongarora, ambaye alivituma kwangu kama kifurushi. Ustadh Ruo Kimani Ruo alikuwa na maktaba nzuri ya kibinafsi. Nilipomtaarifu kuwa nilikuwa natapatapa kutafuta vitabu hivyo, ambavyo havipatikani ‘kwa urahisi’, alifanya ihsani ya kunigutua kuwa alikuwa navyo, na kukubali kunisaidia. Ajabu ni kwamba, sikuwahi kukutana naye ana kwa ana, ingawa tuliwasiliana mara kwa mara, palipokuwepo na haja. Kimefiwa Kiswahili. Kiswahili kimefiwa.”
Prof Kineene wa Mutiso: “Makiwa kwa familia na marafiki zake. Hayati alikuwa mtu wa watu, mpole, mtafiti, mpenzi wa Kiswahili na mzalendo. Hakika, maisha yetu hayatabiriki.”
Mwandishi Henry Indindi: “Kiswahili kimefiwa! Tunamwombea Mzee Ruo Kimani Ruo pumziko la amani. Jina lake na mchango wake katika Kiswahili ni alama ya kudumu.”
Prof Mwenda Mbatiah: “Makiwa kwa jamaa na marafiki wa Ruo Kimani Ruo. Kiswahili kimefiwa sana.”
Dkt Nancy Ngowa: “Pole sana kwa familia yake. Mwalimu Ruo alikuwa msimamizi wangu katika Shule ya Aga Khan Academy, Nairobi nikiwa katika mazoezi ya kufundisha (Teaching practice). Alikuwa mwalimu mzuri sana. Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.”

Dkt Mutahi Miricho: “Pole kwa familia na marafiki za Ruo Kimani Ruo. Namkumbuka Ruo Kimani kama mtu aliyejitahidi sana kukuza Kiswahili kwa kuandika. Nikiwa shuleni nilisoma makala yake kwenye Taifa Leo mara kwa mara. Mungu alaze roho zao pema. Amani kwa familia zote.”
Mwandishi Amina Mlacha Vudzo: “ Sijamini kuwa Mwalimu Ruo Kimani Ruo ametutangulia. Aaa! Ruo alikuwa mkereketwa hali si wa Kiswahili. Tulifanya kazi pamoja ya kukitetea na kukikuza kiswahili kabla ya Karne hii. Alikuwa ni kati ya waalimu wachache wa kiswahili waliochangia kukifanya Kiswahili kuwa somo la lazima nchini. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina Vuzo.”
Soma zaidi: Uhakiki wa tamthilia ‘Mbaya Wetu’
Mwandishi Ali Attas: “Ni pigo kubwa. Sina ziada la kusema maana kifo chake kimenigutusha mno hasa kwa sababu ni hivi majuzi tu nikizungumza naye kwa simu. Mimi ndiye niliyempokeza kazi yangu marehemu Ustadh Ruo Kimani Ruo nilipoacha kufundisha na kujiunga na OUP kama Mhariri wa Kiswahili mnamo mwaka wa 1979. Bado sijaamini kuwa ametuaga.”
Marion Bosire: “Makiwa! Mungu aifariji familia, jamaa na marafiki. Ni pigo kubwa sana kwa Kiswahili.”
Wasifu
Ruo alizaliwa Limuru, Kaunti ya Kiambu, mnamo Agosti 15, 1948, pia alishiriki katika michakato iliyoathiri uimarikaji wa sera ya lugha nchini Kenya. Alisomea Vyuo vya St Mark na St John nchini Uingereza alikojipatia shahada ya Bachelor of Philosophy, kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Exeter alikojipatia shahada ya pili – katika masuala ya elimu.
Uandishi
Aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali za kitaaluma na kiutawala kama kuwa Mkuu wa Idara ya Lugha katika shule za Aga Khan Academy, na katibu wa chama cha Kenya Language Association (1974-1980), Kenya Kiswahili Association (1976-1978), Chama cha Kiswahili cha Afrika (CHAKA) na Mwalimu Kiongozi wa walimu wa Kiswahili, Taasisi ya Elimu [sasa KICD] (1986-1999). Kati ya 1978 -1993, Ustadh Ruo aliandika makala kwenye safu ya Lugha Yetu ya gazeti la Taifa Leo. Baadhi ya vitabu vyake ni: Kiswahili Gold Medal Series (Macmillan, 1991) na Kiswahili Explore Series (Longman, 2003). Ustadh Ruo pia alikuwa mmoja wa wafasiri wa sura za Juzuu la Kwanza ya Mradi wa UNESCO/ TUKI wa kutafsiri ‘Historia ya Afrika’ (1983-1985).
Mipango ya mazishi
Kulingana na familia ya marehemu, atazikwa Desemba 10, 2025 katika eneo la Ihindu, Naivasha, Kaunti ya Nakuru.
Mikutano ya mipango ya mazishi inaendelea katika makazi yake Naivasha, kutoka saa 11:30 hadi saa 2.30 jioni kila jioni.
Kwingineko ni: Nairobi – Parklands Sports Club (Mawingu Room).
Shirika la habari la Newsflash linaitakia jamaa na marafiki wa marehemu uvumilivu wakati huu mgumu.
Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.
