Jalada la tamthilia ‘Mbaya Wetu’. Picha/Maktaba
Mwandishi: Ken Walibora
Mchapishaji: Moran Publishers
Mhakiki: Wanderi Kamau
Kitabu: Tamthilia
Jina la Utungo: Mbaya Wetu
Kurasa: 204
MOJAWAPO ya maovu makuu ambayo yamekuwa yakiizonga jamii yetu kwa sasa ni ufisadi.
Sakata za ufisadi zimefikia kiwango cha kushtua; kila kiongozi wa kisiasa akionekana kuugua saratani hiyo. Hata hivyo, suala hili lina upana mkubwa unaowazidi viongozi wenyewe.
Ni maradhi ya mtikisiko wa kimaadili wa jamii.
Uhalisia huu mchungu ndiyo anaouangazia kwa kina marehemu Prof Ken Walibora katika tamthilia Mbaya Wetu.
Ikiwa tamthilia yake ya kwanza katika orodha ya vitabu zaidi ya 40 alivyoviandika kufikia sasa, msomi huyu amezama kabisa na kudhihirisha kinaya kuwa jamii huwa inamshabikia ‘mtu wao’ licha ya kuwa mbaya.
Mhusika mkuu tamthiliani ni kijana Matari, ambaye ni kitindamimba wa Bw Temba. Matari anasawiriwa kama mkosefu wa maadili, anayeihangaisha jamii yake, kusudi kuu likiwa ni kuwafurahisha marafiki zake, ambao ni walevi.
Ngome ya walevi
Tamthilia inaanza katika eneo moja la walevi, linaloitwa kwa Fiona. Fiona ni mwanamke ambaye huwauzia pombe wanakijiji, ambapo katika onyesho hili wanajadiliana kuhusu athari za pombe ya Fiona—wanayojadili ikiwa inawalewesha ama kuwapofusha. Katika majadiliano yao, inabainika kuwa mbali na kuwalevya, Fiona amekuwa akiwapunja kutokana na bei ghali ya pombe anayowauzia.
Baadaye, anawasili Matari ambaye wanamshangilia. Matari alikuwa mmojawapo wa wateja wakuu wa Bi Fiona. Wanamshangilia kwa kuwa alikuwa akiwanunulia pombe kila wakati akija hapo.
Soma zaidi:Five years on, Ken Walibora’s death remains a mystery
Watu hao wanampa msimbo ‘Matari Kitindamimba Mwana Kindakindaki Mburumatari bin Hatari bin Temba’ ili kumfurahisha awanunulie pombe.
Kwa furaha, Matari anamwagiza Fiona awape pombe watu hao, huku akitoa kibunda cha Sh90,000, inazobainika baadaye kwamba alikuwa ameziiba kutoka kwa dadaye Lila. Muda mfupi baadaye, Lila anafika akiwa na ghadhabu na kumwagiza Matari kumrejeshea pesa zake.
Kabla ya Matari kufika katika eneo hilo, watu hao walikuwa wakimsema vibaya, ambapo wanageuza mkondo wa mazungumzo yao tu pale Fiona anapofika na kuanza ‘kumsifu’ Matari. Kwa hivyo, kinachojitokeza ni kwamba sifa anazolimbikiziwa Matari ni hadaa tupu ili awanunulie watu hao pombe.
Matari anaiba ng’ombe
Ili kuwafurahisha ‘rafikize’ kabisa, Matari anaiba ng’ombe wa Tonge, ambaye ni kakaye. Mbali na hayo, anaiba vipuli vya trekta ya babaye. Kwa hasira, Tonge anawaita polisi ambao wanamkamata Matari na kumzuilia katika kituo chao. Hata hivyo, anashangaa kugundua kiwango cha ufisadi kilichoshamiri miongoni mwao. Polisi wanafasiri visivyo kauli ya ‘Hakuna Kitu Kidogo’—kwamba huwa hawapokei hongo ndogo, bali kiasi kikubwa. Tonge analazimika kuongeza kiwango cha pesa alizokuwa ametoa.
Kinaya ni kuwa wanakijiji wanaandamana wakishinikiza kuachiliwa kwa ‘Mbaya Wao’ licha ya maovu aliyokuwa ametenda.
Soma zaidi: Kiswahili fraternity mourns Prof John Habwe
Wanasema kwamba kulikuwa na ‘ombwe kubwa’ siku kadhaa ambazo Matari alikuwa amezuiliwa. Wanazua vurumai kwa kiasi cha polisi kufyatua risasi hewani. Hata hivyo, hilo haliwazuii hata kidogo kudai kuachiliwa kwa “Mbaya Wao”—Matari.
Kwa ujumla, kinachojitokeza katika tamthilia hii ni kuwa msingi wa maovu katika jamii umetaasisika katika nafsi za raia wenyewe. Kwa mfano, mamaye Matari anasisitiza kwamba hangependa kuona mwanawe akitesekea mikononi mwa vyombo vya dola. Anapendekeza polisi na mawakili kupewa hongo; lengo kuu likiwa kutoteseka kwa mwanawe. Anamtetea Matari kwa kila hali.
Watetea haki ni ‘wasaliti’
Kinaya kikuu katika tamthilia hii ni kuwa wanaojaribu kutetea haki wanaonekana kuwa ‘wasaliti’ wa jamii na msingi wake, ambao umejengeka katika nyenzo za hadaa na ufisadi.
Kwa mfano, mamaye Matari anamshutumu sana bintiye, Lira, anayesisitiza kwamba lazima achukuliwe hatua za kisheria ili kumlainisha kimaadili. Tonge vile vile anakabiliwa vikali na Mzee Temba pale anaposisitiza kwamba lazima Matari achukuliwe hatua kwa kumwibia ng’ombe wake.
Soma zaidi: SAFAL Kiswahili Prize unveils 2024 shortlist
Licha ya kuwa Matari anahukumiwa kifungo cha miaka ishirini na mahakama kwa kumwibia na kumbaka Fiona, kilicho wazi ni kwamba jamii imechorwa kuyashabikia maovu na kuubeza ukweli.
Uhalisia huu ndiyo ulio katika mataifa mengi ya Kiafrika, ambayo yamejipata mikononi mwa watawala madikteta na wafisadi. Mwandishi amefanikiwa sana kutumia mbinu kama kinaya, lugha fiche, methali, kati ya nyingine, kuteka hisia za msomaji.
Tamthilia hii ni muhimu sana kwa kila mmoja katika jamii, hasa katika kuwapa mwanga wananchi kuhusu maovu yanayowaathiri, na hivyo basi ni tamthilia zinduaji.
